YANGA imevuliwa taji la pili msimu huu, baada ya kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inayojulikana kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kufuatia kipigo cha 1-0 kutoka kwa Mbao FC katika mchezo wa Nusu Fainali jioni ya leo Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Mapema mwanzoni mwa msimu, Yanga ilivuliwa taji la Ngao ya Jamii baada ya kufungwa na Azam FC kwa penalti 4-1 kufuatia sare ya 1-1 katika mchezo wa kuashiria ufunguzi wa msimu mpya, Agosti 17, mwaka jana. Na sasa Yanga ina jukumu la kutetea taji lake moja lililobaki na kubwa zaidi, la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ambako wanakabana koo na wapinzani wao wa jadi, Simba SC. Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Erick Onoka wa Arusha, aliyesaidiwa na Julius Kasitu na Mdogo Makame wa Shinyanga hadi mapumziko, tayari Mbao walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0.Ni Yanga wenyewe waliojifunga bao hilo dakika ya 27, baada ya beki wake, Andrew Vincent ‘Dante’ kuunganishia nyavuni kwake kros...