WAZIRI MHAGAMA AKABIDHI VIFAA VYA KUTEMBELEA KWA WALEMAVU
Na Charles James wa Michuzi TV
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Ulemavu Jenista Mhagama amesema Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu na kuhakikisha wanapata huduma bora zinazowahusu bila changamoto yoyote.
Waziri Jenista ameyasema hayo wakati akikabidhi vifaa vya kutembelea Baiskeli 'wheelchair' na fimbo kwa watu wenye ulemavu mkoani Dodoma.
" Niwapongeze sana Kampuni ya Sigara nchini TCC kwa kuandaa tukio hili sambamba na kugawa vifaa hivi maalumu vya kutembelea kwa ndugu zetu wenye ulemavu.
" Hii ni kumuunga mkono Rais wetu Dk John Magufuli katika kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu ambapo tumeshuhudia katika Serikali yake akiteua watu wenye ulemavu kushika nafasi mbalimbali," amesema Waziri Jenista.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia watu wenye Ulemavu, Stella Ikupa amemshukuru Waziri Jenista kwa kukubali kuwa mgeni rasmi kwenye tukio la makabidhiano ya vifaa hivyo kwani imeonesha jinsi gani Serikali inathamini watu wenye ulemavu.
Nae Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Kazi ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde ameupongeza Uongozi wa TCC kwa kugawa vifaa hivyo kwa wananchi wake kwani vitawarahisishia majukumu yao.
" Niwashukuru sana TCC mmekua wadau wakubwa katika kuwashika mkono ndugu zetu wenye ulemavu, mara kwa mara mmekua mkitoa misaada ambayo imekua pia ni chachu ya kukuza vipato vyao," amesema Mavunde.
Mkurugenzi wa Sheria wa Kampuni ya TCC, Godson Kiliza ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwasaidia watu wenye Ulemavu ikiwa ni pamoja na kuwapa vifaa hivyo vya kutembelea pamoja na nyenzo za biashara.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia watu wenye Ulemavu, Stella Ikupa(katikati)akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watu wenye ulemavu baada ya kupatiwa vifaa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Ulemavu Jenista Mhagama akizungumza Mjini Dodoma wakati akikabidhi vifaa vya kutembelea Baiskeli 'wheelchair' na fimbo kwa watu wenye ulemavu mkoani Dodoma.
Waziri Mhagama akikabidhi fimbo kwa moja ya watu wenye ulemavu Jijini Dodoma
Comments
Post a Comment