Wanaoiga nembo kusakwa


Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, amekitaka Kiwanda cha kuunganisha magari cha Rajinder kuwasilisha malalamiko ya baadhi ya watu kuiga teknolojia yao kwa maandishi kwa Tume ya Ushindani nchini (FCC).

Alisema waigaji hao wanaodaiwa kughushi na kutumia nembo ya Rajender,  taarifa zao zikifikishwa kwa maandishi watashughulikiwa kwa wakati.

Aliyasema hayo jana wakati alipotembelea kiwanda hicho na kuwataka waandike barua rasmi  ili serikali iweze kushughulikia malalamiko hayo na hatua kali za kisheria zichukuliwe.

“Naiagiza tume ya usimamizi kuhakikisha inafika katika kiwanda cha Rajender na kushughulikia malalamiko hayo, ili kutokomeza na kudhibiti watu wasio waaminifu wanaotumia nembo ya Rajinder,” alisema na kuongeza kuwa

“Hatutamvumilia mtu yeyote atakayemsababishia mwekezaji hasara ya  kufunga kiwanda chake kwa ajili ya watu ambao si waaminifu wanaonakili na kukopi nembo ya mtu anayelipa staiki zote za serikali…”alisema.

Aliahidi kuwa serikali itamchukulia hatua kali za kisheria ili kutokomeza tabia hiyo.

Aidha, Waziri Kakunda alikitaka kiwanda hicho kusimamia usalama wa watu kazini ili kuepuka mamlaka zilizopo kuwapa adhabu.

“Pamoja na utendaji wenu mzuri unaofanyika naomba mzingatie zoezi la usalama kazini kwa wafanyakazi na utunzaji wa mazingira ikiwa ni hatua mojawapo ya ufanisi,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Manmohan Bhamva, alisema kinakabiliwa na changamoto kubwa ya watu kuigiza anachofanya huku akiiomba serikali kuangalia namna ya kutokomeza changamoto hiyo ili aweze kupanua kiwanda chake katika maeneo mbalimbali ndani na  nje ya nchi.





from MUUNGWANA BLOG

Comments

Popular posts from this blog