BORA MONDI WA MBAGALA KULIKO WA MADALE
WANAOUCHEZEA muziki wa Bongo Fleva hawajui historia yake na hawawafahamu waliotoka jasho na damu kuufanya ukubalike na uwe biashara.
Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ anayetamba kwa mafanikio anapita kwenye barabara ya kimuziki iliyochongwa na kuwekwa lami kwa tabu na Saleh Jabir ambaye kwa mara ya kwanza, mwaka 1991 alirekodi wimbo wa kwanza wa Hip Hop kwa lugha ya Kiswahili.
Kwa Jabir haikuwa rahisi kwa wimbo wake wa kwanza uitwao Ice Ice Baby ambao unaweza kusema ndiyo baba wa nyimbo zote za Bongo Fleva, kukubalika kwenye jamii kama nyimbo za siku hizi zinazopata viewers wengi siku ya kwanza tu kutoka.
Diamond na wasanii wengine wa Bongo wanapojaribu kuufanya muziki wa Bongo Fleva uonekane tena ni wa kihuni kwa kutunga baadhi ya nyimbo zenye maudhui ya matusi wanakuwa wanahujumu harakati za kina Nigga One, Eazy B, D Rob, KBC Kibacha, Y Thang, Killa B na II Proud ambao waliitwa wahuni kwa sababu ya muziki wa Bongo Fleva. Kwa sababu ya fikra za UHUNI nyimbo za Bongo Fleva enzi hizo hazikupigwa kwenye vituo vya redio na marufuku kubwa ilikuwa kwa wazazi na walezi.
Miaka hiyo ya mapinduzi ya fikra za kuufanya muziki wa Bongo ukubalike; kijana kusikika akiimba wimbo wa Bongo Fleva ilikuwa ni ishara tosha kwenye jamii kwamba ameanza kutumia ‘mmea’ na kwamba akili yake imeshaingiwa virusi.
Lakini pamoja na kuitwa wahuni, watu wa ovyo na vijana waliochanganyikiwa kimaisha na kukosa maadili, wasanii wa enzi hizo hawakukata tamaa, waliendelea kuamini kwamba sanaa yao si ya kihuni bali ni njema kama nyingine.
Makundi yalipoanzishwa miaka ile ya 1994 na kuendelea yalianza kupindua meza kibabe, waliokuwa wagumu kuukubali muziki wa Kibongo walianza kulainika. Kundi la Kwanza Unit ambalo lilifyatua wimbo wake wa kwanza uitwao Tucheze, lilichagiza safari ya kuelekea kuufanya muziki wa Bongo Fleva kuwa si wa kihuni.
Mwanga huo wa kukubalika kwenye jamii ulikuwa ni njia sahihi iliyofuatwa na makundi mengine kama Hard Blasters Crew ambao walitoa wimbo uitwao Mambo ya Mjini.
Mr II au Sugu ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Mbeya Mjini anajulikana kwa jina la Joseph Mbilinyi alisimama kama msanii wa kujitegemea na kutoa wimbo alioupa jina la Chini ya Miaka 18. Kwa kuwa si mantiki ya makala haya kuelezea historia ya muziki wa Bongo Fleva, lakini dokezo hizo zilikuwa na maana ya kuweka kumbukumbu sawa kwamba safari ya kujinasua kutokana kuitwa muziki wa kihuni na kuwa wa kistaarabu haikuwa rahisi.
Ugumu huu siusemi mimi, lakini Watangazaji na Madj waliojitoa mhanga kubeba jukumu la kupiga nyimbo za Bongo Fleva enzi hizo kama Taji Liundi, Mike Mhagama, Ibony Moalim na Dj John Dilinga wanaelewa zaidi ninacho-andika. Lakini ni ukweli ulio wazi kwamba msoto wa msanii wa zama hizi haulingani na wa zamani kwa sababu hali imeshageuka.
Wasanii wa zamani hawakuwa na nafasi ya kusilizwa hata kama wangetunga wimbo wenye mashairi matamu kama asali. Nafasi haikuwa wazi na ulimwengu ulikuwa gizani. Leo hii dunia imefunguka, ndiyo maana hata nyimbo za ovyo kama “NYEGEZI” na nyingine zilizojaa matusi zinasikika mitandaoni kila mahali.
Kosa kubwa lililowagharimu wasanii wa zamani mpaka jamii ikanyimwa nafasi ya kuwasikiliza ni mtazamo wa kuwa nyimbo zao ni za kihuni pamoja nao. Jasho walilovuja wasanii wa zamani lilikuwa ni kujisafisha na uchafu huo, mpaka leo imefika mahali Bongo Fleva hata waheshimiwa wanaimba na kucheza, maana yake ni kwamba dhambi imetakasika.
Cha kushangaza ambacho ndicho kimenisukuma niandike makala haya ni kuona kuna baadhi ya wasanii wanataka kufanya mapinduzi haramu.
Kwa makusudi au kwa ujinga kuna baadhi ya wasanii wanaamua kuuchafua muziki wa Bongo Fleva ili urudi kwenye UHUNI ulikotoka. Mavazi wanayovaa ya ovyo, nyimbo wanazotunga ni ovyo, maisha wanaoishi baadhi ya wasanii ni ya ovyoovyo na wengi wameishia kuwa mateja.
Kama hayo yote hayatoshi, wanatunga mpaka nyimbo zenye matusi ili kuzidi kutengeneza taswira mbaya kwenye jamii. Muziki wa Bongo Fleva uonekane ni wa kihuni. Wimbo uliomtoa Diamond kimasomaso ni Mbagala. Hakika ilikuwa ni kazi nzuri iliyomfanya apae kimuziki na kuonekana ni kijana anayetunga nyimbo zilizokwenda shule.
Lakini ukifuatilia Diamond wa Mbagala wa enzi hizo ni ‘mtamu’ zaidi ya huyu wa Madale anayetungatunga nyimbo nyingine zenye ukakasi na kuishia kufungiwa. Sitaki kumsema sana Diamond kwa sababu sikumlenga yeye, lakini kwa ukubwa wake amebeba taito ya makala haya ili nifikishe ujumbe wangu vizuri.
Hata kama wasanii wa Bongo Fleva wataona bado wamesimama na kwamba muziki wao ni msafi mbele ya jamii, ukweli ulio wazi ni kwamba muziki wa Bongo Fleva umeshaanza kunuka. Unanuka kwa sababu wanachanganya mno na kazi za sanaa ‘zilizooza’, matokeo yake jamii imeanza taratibu kuupa kisogo. Kinachosubiriwa ni staili nyingine ya muziki ili Bongo Fleva ife kama dansi ilivyokufa kifo cha mende.
Ni vyema tukumbushane; ni bora Diamond na wasanii wenzake wangechezea fedha wanazopata kwenye kazi kuliko kuchezea kazi inayowapa fedha. Hivi bila muziki Diamond ni nani? Bila sanaa, Nay wa Mitego nani anamfahamu? Ali Kiba, Nature, Jux, Vanessa, Harmonize, Rich Mavoko, Mrisho Mpoto, Darasa na wasanii wengineo, ukiacha muziki utawataja kwa lipi?
Mbona jibu liko wazi; inashindikana nini kazi kuheshimiwa na yenyewe iwaheshimu wasanii wetu? Nawatolea wito wasanii wa Bongo, waamke kuipigania sanaa yao kwa sababu inakoelekea siko; wengi wanaipotea. Mti ukiukata mizizi hunyauka taratibu bila kuonesha dalili. Naiona mizizi ya muziki wa kizazi kipya inaanza kukatwa na tungo za matusi na ubunifu duni.
from SALEH JEMBE
Comments
Post a Comment