SIMBA KAMILI KUTUA ZANZIBAR Klabu ya Simba SC, inatarajia kusafiri Jumatano ya wiki hii ya tarehe 2/01/2019 kuelekea Visiwani Zanzibar kwaajili ya michuano ya kombe la Mapinduzi itakayoanza hivi karibu. Kulingana na taarifa iliyotolewa na uongozi wa Simba mapema leo, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara watatumia michuano hiyo kama sehemu ya maandalizi ya mchezo wao wa ligi ya mabingwa dhidi ya JS Saoura utakaopigwa Jumamosi ya January 12 2019. ZAIDI SOMA HAPA CHINI

Klabu ya Simba SC inatarajiwa kuondoka Jumatano ya January 2, mwakani kwenda Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, ikiwa na kikosi chake kamili.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara amewaambia Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam kwamba watakwenda na kikosi kamili ili kufanya vizuri kwenye mashindano hayo.

Manara, mtoto wa mchezaji nyota wa zamani wa Yanga, Sunday Manara ‘Computer’ amesema pamoja na dhamira ya kufanya vizuri, lakini pia wanataka kutumia michuano hiyo kuipa mazoezi timu yao ambayo inajiaanda na mechi yake ya kwanza ya Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura ya Algeria.

Amesema kuwa mechi dhidi ya timu hiyo mpya ya mshambuliaji Mtanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu itapigwa Jumamosi ya January 12, Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kuanzia Saa 10:00 jioni.

Manara amesema kwamba kikosi cha kwanza kitarejea Dar es Salaam mapema hata Simba ikifuzu kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo dhidi ya JS Saoura na kikosi cha pili kitabaki Zanzibar kumalizia michuano hiyo.

“Na kwa kuwa fainali ya Mapinduzi hufanyika January 13, iwapo Simba itafuzu basi kuna uwezekano mkubwa wa baadhi ya wachezaji kurejea visiwani Zanzibar kucheza fainali hiyo,”amesema Manara na kuongeza;

“Ikumbukwe Simba inathamini sana Mapinduzi hayo matukufu na ndiyo maana tumeamua kupeleka kikosi kamili ili kuwapa burudani Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla, licha ya kukabiliwa na mechi ngumu ya kimashindano ya ligi ya Mabingwa barani Afrika,”.

Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2019 imepangwa kuanza kesho, January 1 hadi 13, mwakani ikifanyika katika miji ya Pemba na Unguja ikishirikisha timu tisa.

Timu hizo ni KVZ, KMKM, Jamhuri, Chipukizi, Mlandege na Malindi kutoka Zanzibar na Azam, Simba na Yanga za Tanzania Bara.

Kundi A linajumisha timu za Chipukizi, Mlandege, KMKM na Simba wakati Kundi B litakuwa na timu za KVZ, Malindi, Jamhuri, Azam na Yanga na kama ilivyo kawaida, mechi zote za mashindano hayo zitaonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam kupitia chaneli zake mbalimbali.

Bingwa wa Mapinduzi 2019 atajipatia kitita cha Sh. Milioni 15, ambazo ni ongezeko la Sh. Milioni 5 kutoka zawadi za mwaka huu, Mshindi wa pili atapata Sh. Milioni 10 badala ya Milioni 5 za msimu uliopita.

Mechi zote za mashidano hayo msimu huu zitafanywa Uwanja wa Amaan uliopo Unguja hadi Nusu Fainali wakati mchezo wa Fainali utafanyika Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba.
Mechi za Amaan zitakuwa zinachezwa kuanzia Saa 10:15 jioni na Saa 2:15 usiku huku mechi ya fainali ikitarajiwa kuchezwa kuanzia Saa 9:30 Alasiri.

Simba SC itafungua dimba na Chipukizi January 4, kabla ya kumenyana na KMKM na kumalizia na Mlandege Januari 8, mechi zote zikanzia Saa 2:15 usiku.

Ikumbukwe Simba pia imepangwa Kundi D pamoja na JS Saoura ya Algeria, AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Al Ahly ya Misri katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Kundi A limezikutanisha timu za na Lobi Stars ya Nigeria, Wydad Casablanca ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Kundi B linaungwa na FC Platinums ya Zimbabwe, Horoya A.C ya Guinea, Esperance ya Tunisia na Orlando Pirates ya Afrika Kusini, wakati Kundi C limezikutanisha Ismailia FC ya Misri, CS Constantine ya Algeria, Club Africain ya Tunisia na TP Mazembe ya DRC.

Mechi za hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa zitaanza Januari 11 mwakani na kufikia tamati Machi 17. Droo ya Robo Fainali itafanyika Machi 23, 2019.

Simba SC wataanzia nyumbani January 11 dhidi ya J.S. Saoura kabla ya kusafiri kuwafuata AS Vita January 18 mjini Kinshasa na Al Ahly February 1 mjini Cairo kukamilisha mechi za mzunguko wa kwanza.
Mzunguko wa pili itaanzia nyumbani February 12 dhidi ya Al Ahly Jijini Dar es Salaam, kabla ya kusafiri kuwafuata J.S. Saoura nchini Algeria Machi 8 na kurejea nyumbani kumalizia na AS Vita Machi 15.

Install Application ya Nijuze Habari Uweze Kupata Habari Kama Hizi Kirahisi Zaidi

=>BOFYA HAPA KUINSTALL/DOWNLOAD

Comments

Popular posts from this blog