KAMATI YA RUFAA KUAMUA HATMA YA WAGOMBEA YANGA

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Yanga, Kamati ya Rufaa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inatarajiwa kukutana Januari 4, kusikiliza rufaa za wagombea wawili kisha baada ya hapo kubandika majina rasmi ya wagombea.

Wagombea wawili katika nafasi mbili tofauti wamekata rufaa kutokana na kuenguliwa ambao ni Yona Kevela ambaye alichukua fomu ya kugombea nafasi mbili tofauti, ya uenyekiti na makamu pamoja na Leonard Marango aliyekuwa akiwania nafasi ya ujumbe.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliwaengua wagombea hao kutokana na kushindwa kutimiza vigezo wakati wa kipindi cha usajili. Akizungumza na Championi Jumatatu, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Malangwe Mchungahela, alisema baada ya kusikiliza rufaa hizo, majina yatawekwa hadharani.

“Januari 4 tutakuwa tunasikiliza rufaa za wagombea wawili ambao walikata rufaa kupinga uamuzi uliotolewa wa wao kuenguliwa, baada ya kila kitu kukamilika hapo basi ndiyo tutabandika rasmi majina ya wagombea.

“Uchaguzi unatarajiwa kufanyika Januari 13 na baada ya kubandika majina hayo, wagombea wataendelea kusubiri siku tano kabla ya uchaguzi ndiyo waanze kampeni,” alisema Mchungahela.

Uchaguzi huo wa Yanga unafanyika ili kuziba nafasi ya mwenyekiti, makamu na nafasi tatu za wajumbe wa kamati ya utendaji kutokana na viongozi wa nafasi hizo, Yusuf Manji, Clement Sanga na wengine kujiuzulu.

Install Application ya Nijuze Habari Uweze Kupata Habari Kama Hizi Kirahisi Zaidi

=>BOFYA HAPA KUINSTALL/DOWNLOAD

Comments

Popular posts from this blog