DKT. SHEIN ATOA RISALA YA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi  wa Zanzibar kuendelea kuidumisha hali ya amani na utulivu.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika risala yake ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2019 aliyoitoa kupitia vyombo vya habari, Ikulu mjini Zanzibar.

Katika risala yake hiyo Rais Dk. Shein alieleza kuwa hali ya amani, umoja na mshikamano uliopo nchini ni jambo muhimu linalowavutia Washirika wa maendeleo ambao wanaridhika na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ndio maana wanaiunga mkono katika mipango yake ya maendeleo.

Hata hivyo, Dk. Shein alitoa shukurani nyingi kwa wananchi wote kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuiletea maendeleo Zanzibar ambapo moyo wao huo wa umoja na mshikamano umewezesha kuimarisha vizuri hali ya uchumi wa Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa wakati unakaribishwa mwaka 2019 ni wajibu wa kila Taasisi ya Serikali ikajipima namna inavyoendelea kutekeleza mambo yaliyoagizwa katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015-2020.

Katika risala yake hiyo, Rais Dk. Shein alizitaja kumbukumbu za matukio yalitokea katika mwaka 2018 ikiwa ni pamoja na utiaji wa saini wa Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia (PSA), baina ya Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia na kampuni ya RAK GAS ya Ras Al Khaimah.

Alieleza kuwa mwaka 2018 umefungua milango katika utekelezaji wa dhamira ya kuendeleza kilimo cha mpunga kwa njia ya umwagiliaji maji na utumiaji wa zana za kisasa ambapo tarehe 6 Disemba, 2018 Serikali ilitiliana saini Mkataba wa Ujenzi wa Miundombinu ya Kilino cha Umwagiliaji maji na Kampuni ya Kokon Hansol JV ya Jamhuri ya Korea kupitia Shirika la Maendeleo la nchi hiyo.

Alisisitiza kuwa kwa upande wa Zanzibar inauanza mwaka 2019 ikiwa imejipanga kwa kutafuta njia bora za kutumia rasilimali za bahari kwa kuitumia vizuri bahari ya Hindi iliyoizunguka kwani hili ni eneo muhimu kwa uchumi wa Zanzibar.

Akieleza jambo jengine muhimu ambalo limefanyika katika mwaka 2018, Rais Dk. Shein alisema kuwa tukio linalohusu jitihada za Serikali za kuwakinga wanawake wa Zanzibar na janga la saratani ya shingo ya kizazi ambapo mnamo April 10 Mama Mwanamwema Shein alizindua rasmi Mpango wa Chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Saratani ya Shingo wa Kizazi.

Akimalizia risala yake hiyo, Rais Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wote kushiriki kwa wingi katika shughuli mbali mbali za kuadhimisha miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 zitakazofanyika katika maeneo yao kwani hizo ni sherehe zao kila mmoja ahakikishe anashiriki ipasavyo katika hatua zote.


Install Application ya Nijuze Habari Uweze Kupata Habari Kama Hizi Kirahisi Zaidi

=>BOFYA HAPA KUINSTALL/DOWNLOAD

Comments

Popular posts from this blog