SERENGETI BOYS YAANZA KUUSAKA UBINGWA COSAFA

Timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 'Serengeti Boys' ipo katika maandalizi ya kuelekea mashindano ya vijana ya mataifa yaliyo kusini mwa Afrika 'COSAFA' mwezi Disemba.

Mashindano hayo yatafanyika nchini Botswana ambapo Serengeti Boys inatarajia kushiriki kama mwalikwa. Yatakuwa ni mashindano ya kwanza ya nje ya Afrika Mashariki kwa timu hiyo kushiriki baada ya kumalizika kwa michuano ya CECAFA U-17 Challenge ambayo Serengeti Boys iliondolewa katika hatua ya nusu fainali.

Akizungumza kuelekea michuano hiyo, kocha mkuu wa timu hiyo Oscar Milambo amesema,

"Timu hii toka tumeanza kuijenga hatujawahi kucheza michezo ya kirafiki au ya kimashindano tofauti na ukanda wetu wa Afrika Mashariki na kati, kwahiyo kwa kwenda kucheza kwenye nchi za kusini mwa Afrika tunategemea kwamba tutakutana na changamoto mpya kitu ambacho kitatupa dira ya kuona kwenye maandalizi tumefikia kiwango gani".

"Limekuwa ni jambo la faraja kwamba tumepata nafasi ya kwenda kushiriki kwenye haya mashindano, na kwa sisi waalimu mara nyingi tunaamini kipimo kizuri ni mechi, kwahiyo tunaamini kwa maandalizi tunayoyafanya ni lazima tufanye vizuri", ameongeza.

Ikumbukwe kuwa Serengeti Boys ndiyo wenyeji wa michuano ya mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 mwaka 2019, michuano itakayofanyika hapa Tanzania.

Comments

Popular posts from this blog