NIYONZIMA KIKAANGONI SIMBA SC

Kiungo wa Simba, Mnyarwanda Haruna Niyonzima amewekwa kikaangoni baada ya kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu ya klabu hiyo kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali.

Kwa muda mrefu Niyonzima amekuwa kwenye sintofahamu na mabosi wake huku tangu alipojiunga na wenzake mazoezini hajacheza. Mwanaspoti ambalo lilikuwepo eneo la tukio, limeshughudia kiungo wa huyo na nahodha wa timu ya Taifa ya Rwanda, akitoka kuhojiwa na Kamati hiyo iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Suleiman Kova.

Kova, ambaye amepata kuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, aliongoza kikao hicho akiwa na wajumbe wengine wanne kwenye ukumbi wa hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kuwa Niyonzima aliitwa na kamati hiyo kwa ajili ya kuzungumza masuala ya nidhamu yake huku ikielezwa kuwa pande zote zimeshindwa kufikia mwafaka.

Chanzo chetu ndani ya kikao hicho kimeeleza kuwa, Kamati ya Kova ilikutana na kigingi baada ya kiungo huyo kuonyesha mkataba wake, ambao anadai mabosi wa Simba wameshindwa kutimiza kama walivyokubaliana na kwamba, ndio sababu ya yeye kuonekana mtovu wa nidhamu.

“Ni kweli kama ulivyoona, Niyonzima ameitwa kuhojiwa na Kamati ya Kova, lakini mambo ni magumu sana. Tulimuita kupata ufafanuzi juu ya madai ya kuelezwa kuwa ni mtovu wa nidhamu, lakini makubaliano yake kwenye mkataba na Simba sio ya mchezo mchezo.

“Kama ndio vile, basi ni suala gumu sana kwa Simba kuvunja mkataba wake kwani, kuna mambo mengi ambayo hawajakamilisha mambo mengi ya kimkataba na kama watataka kuuvunja basi watalazimika kulipa pesa nyingi,” kilisema chanzo chetu.

Mwanaspoti lilizungumza na Niyonzima, ambaye alikiri kuitwa na kufanya kikao hicho ingawa hakutaka kuweka wazi masuala yaliyojadiliwa.

“Sivunji mkataba Simba, ila ni kweli tulikuwa na kikao na viongozi humo ndani, nipo Simba na siwezi kuondoka bila kuwafanyia kazi yao. Nilikwenda nyumbani ila nimerudi muda na itacheza Mungu akipenda kwani nipo fiti,” alisema Niyonzima wakati akitoka kwenye kikao

Comments

Popular posts from this blog