KESI INAYOWAKABILI VIONGOZI WATATU WA SIMBA KUANZA KUSIKILIZWA

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kesho Jumatano ya October 31 itaanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya kughushi na kutakatisha fedha inayowakabili viongozi watatu wa Klabu wa Simba.

Washtakiwa hao ni Rais wa Klabu hiyo, Evans Aveva, makamu wake, Geofrey Nyange Kaburu na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.

Hatua hiyo inatokana na upande wa mashtaka kumaliza kuwasomea maelezo ya awali (PH) na hivyo, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, kupanga October 31, 2018 kuanza kisikiliza ushahidi.

Kesi hiyo inatokana na matumizi ya pesa za uhamisho wa mchezaji wa klabu hiyo, Emmanuel Okwi, kwenda Klabu ya Etoile Sportive Du Dahel ya Tunisia, kwa madai ya kutumia pesa hizo kununulia nyasi bandia na gharama za ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo ulioko Bunju.

Katika kesi hiyo Hans Poppe anakabiliwa na mashtaka mawili, kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uongo yeye pamoja na wenzake.

Wakati, Avena na Nyange wanakabiliwa na mashtaka 10 yakiwemo matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha hizo bila mamlaka ya Kamati ya Utendaji ya Simba, kujipatia pesa isivyo halali (Aveva) na utakatishaji fedha.

Washtakiwa Aveva na Nyange wanatetewa na mawakili Nehemia Nkoko na Nestory Wandiba wakati Hans Poppe anatetewa wa Wakili Agostino Shio.

Siku waliposomewa maelezo ya awali,  October 19, 2018, mfanyabiashara Hans Poppe, alikiri mahakamani hapo kuhusika na mchakato wa ununuzi wa nyasi bandia kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo, ulioko Bunju, wilaya ya Kinondoni,  wakati wenzake walikana mashtaka yao yote.

Comments

Popular posts from this blog