WENGER NA HESHIMA YA KIFO CHA MKWAWA.



Na Yego Sholla

Chifu mkwawa wengi tumemsoma kwenye vitabu vya historia wakati tuko shule. Kwangu mimi huyu anabaki kuwa ni moja ya viongozi jasiri kabisa kuwahi kutokea hapa Afrika mashariki na hata kifo chake kimekuwa cha heshima kubwa sana. Kifo ambacho kinapaswa kuwa kama mfano wa hatma ya Arsene Wenger ndani ya Arsenal.

Mkwawa alikuwa ni kiongozi wa kabila la Wahehe aliepingana na utawala wa Wajerumani enzi za ukoloni miaka ya 1800 mwishoni. Aliwapa shida sana ikiwemo kuua askari wengi sana na hata viongozi wao lakini hata pale alipoona amezingirwa hakusubiri akamatwe bali alijifyatulia risasi mwenyewe. Mkwawa hakusubiri auawe au kukamatwa na Wajerumani.

Baada ya yote aliyowafanyia aliamini kuwa ni yeye tu ndio anastahili kuutoa uhai wake. Aliamini kukamatwa kwake ilikuwa ni ishara kuwa ameshindwa hivyo ni bora ajiue mwenyewe na sio wao kumkamata kwani aliona aibu sana. Mpaka leo fuvu lake lipo na anaheshima kubwa.

Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger wengi walipata kumwona akifanikiwa sana kwenye miaka yake 8 ya mwanzo na kiujumla akiwa ameipa timu hiyo mataji 3 ya ligi kuu, 7 ya FA na ngao za jamii 7, na hakika huyu anabaki kuwa kocha mwenye mafanikio zaidi kwenye historia ya klabu ya Arsenal lakini kila lenye mwanzo huwa halikosi mwisho japo hatma huwa zinatofautiana, kuna mwisho mzuri na mwisho mbaya.

Wenger baada ya kukaa miaka mingi na kushindwa kufikia matarajio ya timu ni wazi anapaswa kurudi katika vitabu vya historia Afrika mashariki akamsome chifu Mkwawa.

Wenger atakuwa ameondoka kwa heshima kubwa endapo atatangaza mwenyewe kujiuzulu nafasi ya ukufunzi pale Arsenal kuliko kusubiri kuambiwa, kusubiri mkataba uishe au hata kufukuzwa.

Akisubiri kuambiwa maana yake kuna watu bila shaka watakuwa wamemshinikiza kufanya hivyo, akisubiri mkataba uishe maana yake hakuwa na budi tena hapo na itakuja dhana kuwa pengine tu klabu haikuwa na nia ya kumwongeza mwingine lakini akisubiri afukuzwe ndio itakuwa aibu kubwa na yale mafanikio yake yote yataishia kwa aibu.

Heshima pekee atakayojipa na jambo bora ambalo anaweza kulifanya kwa maslahi ya Arsenal kusonga mbele ni kutoa tamko yeye mwenyewe kuwa sasa inatosha.

Binafsi naamini ataagwa kwa heshima kubwa tu na atakuwa ameondoka mtu alieridhiwa kuliko kusubiri watu au uongozi ndio umwamulie. Hata hivyo ningependa zaidi kuona Wenger akiagwa na kitu. Kitu kwa maana ya kombe.

Mwaka 2013 mara baada ya kutwaa ubingwa wa FA dhidi ya Hull City pale Wembley niliamini kuwa ule ndio ulikuwa wakati sahihi wa yeye kuiacha timu ikiwa na kitu cha kufurahia na kumbukumbu nzuri kwake ya kuondokea halikadhalika na mwaka jana pia dhidi ya Chelsea kwenye shindano hilo hilo na hakufanya hivyo.

Mara hii ana nafasi ya kubeba taji lake la kwanza la Ulaya na atakuwa ameiaga timu vizuri mno akiweza pia kuwakatia tiketi ya klabu bingwa washika mitutu hao lakini shida ni kwamba mzee wangu atataka aendelee kusalia klabuni baada ya hapo. Hata hivyo atwae taji au la ni wazi anapaswa kuondoka tu Arsenal.

Wenger ana mawili, aendelee kusubiri muda umhukumu au atengeneze heshima kwa kuamua mwenyewe kuondoka baada ya miaka 22 ya kuwa kocha mwenye mafanikio ambaye kwa sasa ameshazingirwa na anapaswa kujiua mwenyewe kabla hajakamatwa. Kifo cha Mkwawa ndio mwisho anaostahili Wenger pale Arsenal.Credit haatim Abdul

Comments

Popular posts from this blog

Njia sahihi za kuachana na unywaji wa pombe