UJIO WA FIFA WAACHA NEEMA TANZANIA

Ujio wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA umepita,mkutano mkubwa wa FIFA wa maendeleo ya mpira wa miguu(FIFA Football Executive Summit) umefanyika Tanzania ukiacha mambo mengi mazuri nyuma yake.

Tayari Rais wa FIFA Gianni Infantino, akiwa Tanzania kwenye mkutano huo akaacha ujumbe mkubwa akisisitiza kupingana na masula ya rushwa.

Moja ya mambo aliyoyaacha Infantino ni kufurahishwa kwa namna Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF linavyoendeshwa kwa uwazi kwenye masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya fedha.

Rais wa Fifa Infantino pia amefurahishwa na namna serikali ya Tanzania inavyopingana na masuala ya rushwa.

Aidha akaeleza wazi kuwa mkutano huo mkubwa wa FIFA utafungua milango kwa Tanzania katika masuala mbalimbali.

Infantino hakuacha kusema kumfahamu mshambuliaji na nahodha wa Tanzania Mbwana Samatta anayecheza Genk ya Ubelgiji akisema ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa.

Akiwa nchini Infantino pia alikutana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa na Waziri wa Habari,Utamaduni Sanaa na Michezo Dr.Harrison Mwakyembe.

Katika hatua nyingine Infantino amesisitiza kuwa yeye ni kiongozi wa utendaji na sio maneno na ndio maana tokea ameingia madarakani amekuwa anatenda zaidi ikiwemo ongezeko la timu za Africa kwenye kombe la dunia jambo ambalo huko nyuma lilikuwa linazungumzwa bila kutendeka.

Mkutano wa FIFA ulifanyika Februari 22, 2018 na kushirikisha jumla ya mashirikisho 21 ya mpira ambao ni wanachama wa shirikisho hilo na Ajenda kubwa ilikuwa kujadili namna ya kukuza soka la wanawake,soka la vijana na suala la usajili kwa njia ya mtandao.

Pia moja kati ya mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na kuanzishwa kwa ligi kubwa ya Wanawake .

Wakati huohuo Katibu mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Africa Fatmah Samoura baada ya mkutano huo akatembelea Makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania akapata nafasi ya kuzunguka katika sehemu mbalimbali za TFF ikiwemo ofisi na mradi wa hostel.

Comments

Popular posts from this blog