PAMOJA NA USHINDI ROSTAND AAMBULIA LAWAMA

Licha ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ndanda FC, mashabiki na wanachama wa Yanga wamemlalamikia kipa wao Youthe Rostand kutokana na kiwango anachokionesha.

Ukiachana na Mjumbe wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali, kuanza kumnyooshea kidole kipa huyo, baadhi ya mashabiki wamekuwa wakihoji inakuwaje kiwango cha kipa huyo kinashuka.

Kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo Facebook na Instagram, wapo wale walioandika ni muda sasa wa Ramadhan Kabwili au Beno Kakolanya kupewa nafasi ya kucheza nafasi yake.

Hivi karibuni kipa huyo aliyesajiliwa kutoka African Lyon iliyoshuka daraja msimu uliopita, amekuwa hafanyi vizuri tofauti na alivyokuwa akicheza mwanzo.

Mashabiki hao baadhi wamefikia hatua ya kulishauri hata benchi la ufundi kwa kushawishi litoe nafasi kwa Kabwili ama Kakolanya ambaye hajacheza muda mrefu.

Mbali na lawama hizo kutoka kwa mashabiki na viongozi, benchi la ufundi chini ya Kocha, George Lwandamina, limeendelea kumtumia Rostand kama kipa namba moja wa timu hiyo.

Comments

Popular posts from this blog