TFF YAWEKA WAZI VIINGILIO, TAIFA STARS VS BOTSWANA, 02-09-2017.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetangaza viingilio vya mchezo kati ya Taifa Stars ya Tanzania na Botswana utakaofanyika Jumamosi Septemba 2, mwaka huu.

Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam chini ya utaratibu wa kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) viingilio vitakuwa Sh 10,000 kwa Jukwaa Kuu na Sh 5,000 kwa mzunguko.

Wakati huo huo, Kiungo Taifa Stars, Simon Msuva tayari amejiunga na timu hiyo akitokea Klabu ya Difaa El Jadidah ya Morocco baada ya Shirikisho la Soka Morocco na timu yake kumfanyia mpango wa visa ya muda mrefu iliyomwezesha kusafiri.

Mchezaji ambaye imeshindikana kuja ni Orgenes Mollel wa FC Famalicao ya Ureno. Sababu ni taratibu za ruhusa za kimataifa zinafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria za nchi ya Ureno ambako anacheza soka la kulipwa.

Nyota wengine walikwisha kuripoti ni pamoja na Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Elias Maguli (Dhofar FC/Oman), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya) wakati Farid Mussa wa CD Tenerif ya Hispania anatarajiwa kutua leo.

Wengine ambao wako kambini Hoteli ya Sea Scape iliyoko Kunduchi, Dar es Salaam ni makipa Aishi Manula (Simba SC), Mwadini Ally (Azam FC) na Ramadhani Kabwili (Young Africans).

Pia wamo Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphas Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Salim Mbonde (Simba SC) na Erasto Nyoni (Simba SC).

Viungo ni Himid Mao – Nahodha Msaidizi (Azam FC), Mzamiru Yassin (Simba SC), Said Ndemla (Simba SC), Shiza Kichuya (Simba SC), wakati Washambuliaji ni Raphael Daud (Young Africans), Kelvin Sabato (Azam FC) na Emmanuel Martin (Young Africans).

Katika hatua nyingine, Botswana inatarajiwa kuingia usiku wa saa 3.00 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) na watafikia Hoteli ya Urban Rose iliyoko katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Botswana inayonolewa na David Bright inakuja na wachezaji 18 wakiwamo makipa Mampule masule, Noah Maposa na Antony Gouws.

Walinzi ni Letsweletse, Mosha Gaolaolwe, Simisane Mathumo, Thabang Mosigi, Lesenya Ramorake, Tapiwa Gadibolae na Bokani Leeton.

Viungo ni Alphonse Modisaotsile, Maano Ditshupo, Katlego Masole, Gift Moyo, Segolame Boy, Lemponye Tshireletso, Thero Setsile, Kabelo Seakanyeng,Jackson, Lemogang maswena.

Washambuliaji ni Tumisang Orebonye, Jarome Ramathakwane, Tebogo Sembowa, Hendric Moyo na Boipelo Oaitse.

KIDAO AZUNGUMZIA RATIBA VPL

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Kidao Wilfred ameunda kikosi kazi cha wataalamu wanne wa shirikisho kuangalia upya ratiba ya Ligi Kuu ili kuondoa kila aina ya kero inayoweza kuibuka katikati ya mashindano.

Kidao ambaye ana siku tisa ofisini tangu ashike wadhifa huo, amesema kuna changamoto nyingi sana katika shirikisho, lakini kubwa ni hili ambalo wanafamilia ya mpira wa miguu wamekuwa wakijadili kwa sasa.

Wadau wanajadili suala la ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Kwamba baada ya michezo ya mzunguko wa kwanza tu, ratiba imetangazwa kubadilishwa. Ni kweli imebadilishwa kwa sababu ya kupisha wiki ya kalenda ya FIFA ya mechi ama za ushindani au kirafiki kati ya nchi na nchi.

Amesema kwamba makosa yamefanywa na maofisa wa Bodi ya Ligi Kuu ambayo ndiyo yenye dhamana ya kupanga ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL); Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL).

Maofisa hao ilihali wakijua kwamba kuna wiki ya kalenda ya FIFA, walidiriki kupanga mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Sasa tuchukua nafasi hii kuomba radhi Watanzania hususani wanafamilia ya mpira wa miguu ambao kwa namna moja au nyingine wameghafirishwa na kupanguliwa ratiba.

“Lakini suala hili haliwezi kupita hivi hivi bila hatua na kinidhamu kuchukuliwa. Rais wa TFF Bw. Wallace Karia aliniagiza nimwandikie Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu, Bw. Boniface Wambura achukue hatua za kinidhamu kwa maofisa wote waliohusika na upangaji huo wa ratiba ulioingilia ratiba ya kalenda.

Like Page yetu hapa chini ili uwe wa kwanza kupata habari zetu zote za Michezo na Usajili
Kama una picha,Video au Habari zinazohusu Michezo tutumie WhatsApp namba +255756658100. Sambaza habari hii Facebook, Sambaza Twitter, Sambaza WhatsApp Mshirikishe mwenzako

Comments

Popular posts from this blog