VIRUSI VYAMWONDOA DANIEL STURRIDGE MAZOEZINI
Sturridge ameondoka kwenye kambi ya mazoezi baada ya vipimo vya daktari kuthibitisha kwamba hali yake si nzuri na haweza kuendelea na mazoezi Mshambuliaji wa Liverpool Daniel Sturridge amepaa kurejea nyumbani mapema akiondoka kwenye kambi ya mazoezi ya klabu yake Hispania baada ya kupata maambukizi ya virusi. Nyota huyo, 27, alikuwa sehemu ya kikosi kilichopaa kwenda La Manga kwa ajili ya kufanya mazoezi kwenye hali ya hewa ya joto Jumatano licha ya kulalamika kujisikia mgonjwa kabla ya safari. Kwa mujibu wa Liverpool Echo , Sturridge hakuweza kufanya mazoezi ya siku ya kwanza Alhamisi na baada ya uchunguzi wa timu ya madaktari, uamuzi ulifikiwa kumrejesha nyumbani. Kikosi cha Jurgen Klopp kitabakia Hispania hadi Jumapili na wanatarajiwa kuungana tena na Sturridge mapema wiki ijayo. Reds hawana mechi yoyote ya ushindani hadi watakaposafiri kwenda kuwakabili mabingwa watetezi wa taji la Uingereza Leicester City kwenye mechi ya ligi Februari 27.