LWANDAMINA – UWANJA WETU WA MAZOEZI HAUNA HADHI NINAYOTAKA

SIKU moja baada ya kuanza kibarua chake kipya cha kuinoa klabu ya Yanga, kocha mpya wa mabingwa hao wa soka nchini, George Lwandamina ameonesha kutoridhishwa na ubora wa uwanja unaotumiwa kwa mazoezi wa Chuo cha Polisi Kurasini na kuutaka uongozi kutafuta uwanja mwingine.
Mzambia huyo alianza rasmi kibarua chake Jumatatu, ambapo baada ya kumalizika kwa mazoezi yaliyohudhuriwa na wachezaji 18, aliuomba uongozi kumuonesha viwanja vingine vitatu tofauti ili kuchagua ulio bora tofauti na huo wa Polisi Kurasini.
Lwandamina alisema uwanja huo siyo bora kutokana na mfumo wa soka anaotaka kuwafundisha wachezaji wake, hivyo atafurahi kama uongozi utafanya jitihada za kupata uwanja mwingine ambao utakuwa muafaka kwa kile anachotaka kuwafundisha vijana wake.
“Uwanja huu ni mzuri kwa utulivu, lakini una mapungufu mengi ikiwemo sehemu ya kuchezea kukosa usawa, jambo ambalo linasababisha mpira kudunda dunda na kumpa tabu mchezaji kuumiliki,”alisema Lwandamina.
Kocha huyo alisema anaamini Tanzania kuna viwanja vingi vizuri ukiacha ule wa Taifa, ambao umefungiwa kwa sasa kwa timu hizo za Simba na Yanga, hivyo viongozi watapambana ili kuwatafutia uwanja mzuri ambao utamwezesha yeye na wasaidizi wake kutoa mafunzo mazuri kwa wachezaji wao.
Akilizungumzia hilo, Meneja wa timu hiyo, Hafidh Salehe alisema watalifanyia kazi ombi la kocha huyo na muda si mrefu watalipatia ufumbuzi ili timu hiyo ihamishie mazoezi yake kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.
Siku za nyuma Yanga ilikuwa ikipendelea kufanya mazoezi yake kwenye viwanja vitatu ule wa Uhuru, Gymkhana au Boko Veterani na kutokana na maombi ya Lwandamina pengine uongozi ukapendekeza timu kufanya mazoezi yake moja kati ya viwanja hivyo.
Hata hivyo, Tanzania imekuwa na matatizo makubwa ya viwanja huku klabu kongwe za Yanga na Simba zikiwa hazina viwanja vyao na kubaki kukodisha.

Comments

Popular posts from this blog