SIMBA: Muzamil Yassin aumia Enka
SIMBA SC iko hatarini kumkosa kiungo wake tegemeo, Muzamil Yassin katika mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Stand United Jumatano.
Simba SC watacheza mechi ya pili mfululizo Uwanja wa Kambarage, Shinyanga Jumatano wakati timu yao itakapomenyana na Stand, ikitoka kushinda 3-0 dhidi ya Mwadui juzi.
Na Daktari wa Simba SC, Yassin Gembe amesema kwamba Muzamil aliumia kifundo cha mguu juzi katika mchezo na Mwadui.
Muzamil Yassin (kushoto) aliumia kifundo cha mguu katika mchezo dhidi ya Mwadui, lakini leo anatarajiwa kufanya mazoezi
Lakini Gembe alisema kwamba maumivu ya Muzamil aliyesajiliwa Simba SC msimu huu kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro hayatarajiwi kuwa makali ya kumuweka nje muda mrefu.
“Aliumia enka, lakini hatutarajii yawe maumivu makali sana. Nadhani Jumatatu ataweza kufanya mazoezi baada ya mapumziko ya saa 24,”alisema.
Gembe alisema majeruhi ambaye ataendelea kuwa nje ya programu za timu ni mshambuliaji Muivory Coast, Frederick Blagon ambaye amebaki Dar es Salaam kwa matibabu.
Gembe alisema kwamba Blagnon baada ya wiki moja ya mapumziko, atahitaji tena japo siku tatu za kufanya mazoezi ili kuwa fiti - maana yake atakuwa a jumla ya wiki zisizopungua mbili za kuwa nje tangu aumie wiki iliyopita kwenye mechi na Toto Africans Simba ikishinda 3-0 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment