Viungo Simba, Yanga kuamua matokeo
Mara nyingi ukifuatilia historia ya michezo ya mahasimu wa mji mmoja ‘Derby’ baina ya Simba na Yanga, matokeo ya mchezo huo mara nyingi huamuliwa na ufundi unaooneshwa eneo la kati la Uwanja
Ubora wa wachezaji wanaocheza eneo hilo la uwanja, ‘Midfielders’ huweza kuamua matokeo kwa timu katika mchezo huo kutokana na aina ya washambuliaji waliopo katika timu zote mbili na mifumo wanayotumia.
Mathalani, wachezaji kama Jonas Mkude, Mzamiru Yassini, Said Ndemla na Mohamed Ibrahim ndiyo unaofanya Simba kuonekana kuwa na utulivu na kuifanya timu hiyo imiliki mpira kwa muda mrefu huku ikitengeneza nafasi nyingi za kufunga kutokana na viungo hao kupiga pasi nyingi kuelekea eneo la wapinzani.
Inaweza kuwa tofauti kidogo kwa Yanga katika mfumo wa uchezaji kwa ujumla, hata hivyo ubora wa viungo si tofauti sana kutokana na Yanga kutokuwa na kawaida ya kumiliki mpira muda mrefu licha ya kuwa na viungo wazuri kama Haruna Niyonzima na Thaban Kamusoko.
Niyonzima na Kamusoko wana uwezo mkubwa wa kukaa na mpira kwa muda mrefu.
Simba inaweza kuwa na faida kutokana na Kocha wao kuwa na tabia ya kutumia viungo watatu mpaka wanne kutokana na aina ya timu wanayocheza nayo, huku wakiwa na tabia ya kukaa na mpira muda mrefu huku wakitengeneza mashambulizi polepole, kitu ambacho kinaweza kuwapa wakati mgumu Yanga kutumia muda mwingi kuzuia kuliko kushambulia.
Yanga wanaweza kuimudu hiyo hali endapo kocha wao Hans Van Plujim, ataamua kuingia katika mchezo huo kwa kutumia wachezaji watatu katika eneo la katikati ya uwanja ambao ni Niyonzima, Kamusoko na Mbuyu Twite ambaye atacheza mbele ya mabeki wanne kwa kazi ya kuzuia zaidi.
Silaha nyingine, anayoweza kutumia Plujim kuiadhibu Simba ni kuamuru viungo wake kutengeneza mashambulizi kupitia pembeni ya uwanja kwa kuwatumia Simon Msuva, Deusi Kaseke na Donald Ngoma ambaye naye huwa na tabia ya kushambulia kutokea pembeni kutokana na kuwa na kasi kubwa.
Kwa uchambuzi kuhusu ubora wa safu ya ushambuliaji kwa timu zote mbili na namna gani safu hiyo inaweza kubadilisha matokeo ndani ya uwanja katika mchezo wa Jumamosi, usikose kusoma MwanaHALISI Online siku ya kesho kwa uchambuzi zaidi.
Comments
Post a Comment