Tetemeko lang’oa vigogo 3 Kagera
* Walifungua akaunti feki ya michango ya waathirika
RAIS Dk. John Magufuli, ametengua uteuzi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera (RAS), Amantius Msole na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Steven Makonda, baada ya kubaini wamefungua akaunti nyingine ya benki kwa kutumia jina linalofanana na akaunti rasmi ya kuchangia maafa iitwayo “Kamati Maafa Kagera” kwa lengo la kujipatia fedha.
Uamuzi huo, umekuja siku 10 baada ya Rais Dk. Magufuli kuonya na kuvitaka vyombo vya dola kuwafuatilia watu wanaotaka kutumia maafa hayo kukusanya michango kwa lengo la kujinufaisha.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo, Septemba 17, mwaka huu Ikulu, jijini Dar es Salaam wakati akipokea taarifa ya maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera kutoka kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais ameagiza vyombo vya dola vichukue hatua dhidi ya watu wote waliohusika katika njama za kufungua akaunti hiyo.
Taarifa hiyo, ilisema Rais Dk. Magufuli alitoa uamuzi huo, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri Mkuu Majaliwa muda mfupi baada ya kupokea hundi ya msaada kutoka kwa Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa naye amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Simbaufoo Swai kutokana na kuhusika katika njama hizo.
Comments
Post a Comment